Marekani kuongeza majeshi Ulaya

Haki miliki ya picha n
Image caption Baadhi wanataka Marekani kuwa na wanajeshi wa kudumu Ulaya

Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza mpango wa dola bilioni moja kufadhili nyongeza ya wanajeshi wake barani Ulaya huku mzozo wa Ukraine ukiendelea kutokota.

Obama ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya Poland.

Bwana Obama atakutana na viongozi wa Ulaya baadaye Jumanne kujadili kuhusishwa kwa wanajeshi wake katika mpango wa ulinzi katika kanda hiyo.

Kadhalika Obama amesisitiza kuwa kujitolea kwa Marekani katika harakati za ulinzi Mashariki mwa Ulaya ni njia yake ya kutaka kusaidia kuhakikisha ulinzi unaimarishwa barani humo.

Ikulu ya White House imesema kuwa pesa hizo zitafadhili shughuli za jeshi la Marekani katika kanda hiyo, hususan mpango wa Marekani kuongeza wanajeshi katika shirika la ulinzi la NATO.

Pia Obama amesema kuwa hilo bila shaka halitazuia Marekani kujitolea kwa maswala ya usalama katika eneo la Asia ya Pacific.

Image caption Obama na akiwa nchini Polanda kwa mazungumzo na Rais wa Poland Bronislaw Komorowsk

Mgogoro wa Ukraine, umeathiri pakubwa eneo hilo ambalo lilitawaliwa na Urusi kwa miaka mingi.

Baadhi ya nchi kama Poland, zingependa kuona Marekani ikiwa na jeshi la kudumu katika kanda hilo.

Bila shaka pendekezo hilo halijatolewa lakini ikiwa litatolewa bila shaka litapokelewa kwa mikono miwili.

Obama pia atazuru Ubelgiji na Ufaransa wakati wa ziara yake Ulaya.

Wakati huohuo, mawaziri wa ulinzi wa Nato, wanatarajiwa kukutana mjini Brussels kujadili athari za muda mrefu zitakazosababishwa na vitendo vya Urusi nchini Ukraine.

Ikulu ya Urusi imekanusha madai kuwa inaunga mkono wapiganaji wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine.