Ujerumani kuchunguza madai ya udukuzi

Image caption Obama amesema amesikitishwa na kudorora kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili

Ujerumani inachunguza madai yaliyotolewa na mtoro mmarekani, Edward Snowden kuwa Marekani ilifanyia udukuzi simu ya Chansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Mwendesha mkuu wa mashitaka wa Ujerumani,Harald Range, alifahamisha kamati ya kisheria ya bunge la ujerumani kuwa uchunguzi utafanywa dhidi ya watu ambao hawakutajwa.

Bi Merkel ametaka ufafanuzi kuhusu madai hayo ambayo yanahusisha shirika la ujasusi la Marekani (NSA).

Jopo litakaloendesha uchunguzi huo, ilitangazwa wakati wa ziara ya Rais Obama barani Ulaya.

Wakati huohuo, Bwana Range amesema kuwa aliamua kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya shirika la NSA kupeleleza wananchi wa Ujerumani.

'Machungu'

Viongozi wa Ujeruami na Marekani, wanatarajiwa kukutana mjini Brussels katika mkutano wa G7.

Rais Obama alimwambia Merkel mwezi jana kuwa alihisi uchungu mwingi kwamba ufichuzi wa Snowden umeathiri pakubwa uhusiano kati ya mataifa hayo.

Rais Obama amesema kuwa amewaamuru maafisa wake wa ujasusi kuchunguza uzito wa udukuzi dhidi ya raia wa Marekani na kuzingiatia swala la usiri wa maisha yao.

Merkel amependekeza kuanzisha mtandao wa mawasiliano wa Ulaya kuzuia ujumbe wa faragha wa maafisa ulaya kufikiwa na Marekani.