G7 watishia kuiwekea Urusi vikwazo zaidi

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mkutano wa G7

Viongozi wa mataifa tajiri ya magharibi wanaokutana mjini Brussels wamesema kuwa wako tayari kuweka vikwazo zaidi kwa Urusi iwapo itaendelea kuvuruga amani mashariki mwa Ukrain.

Taarifa ya pamoja ya mataifa ya G7 imesema kuwa Mambo yanayofanywa na Urusi nchini Ukrain hayawezi kukubalika kamwe na lazima yakomeshwe.

Huu ndio mkutano wa kwanza wa viongozi hao tangu waifukuze Urusi kama mwanachama.

Urusi ilibumburushwa kutoka G7 kwa kosa lake kubwa zaidi, kuinyakua Crimea kutoka Ukraine.

Viongozi wa mataifa hayo ya G7 wanakutana sasa kwa mara ya kwanza tangu wakati huo.

Lakini huku wakikutana mapigano yamechacha kati ya serikali ya Ukrain na majeshi yanayounga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine.

Urusi imeendelea kukana kuhusika na mapigano hayo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ukraine vita vimechacha

Miongoni mwa mikutano iliyopangwa Alhamisi hii, waziri mkuu wa Uingereza Davin Cameron atakutana na rais Obama mjini Brussels, ambapo kwa upana zaidi watazungumzia Urusi.

Kisha baada ya mkutano huo, David Cameron ataelekea Paris Ufaransa kwa mkutano wa faragha na rais wa Urusi Vladmir Putin.

'D-Day barani Uropa'

Katika wiki hii mataifa ya Uropa yamekuwa yakiadhimisha siku ya kuikomboa bara Uropa kutoka utawala wa ki Nazzi katika vita vya pili vya dunia miaka 70 iliyopita.

Huku hayo yakitokea, juhudi za kidiplomasia zimeshika kasi miongoni mwa mataifa ya magharibi kumaliza uhasama kati yao na Urusi.

G7 wamepongeza uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Ukrain na wameirai Urusi kumpokea na kushirikiana na rais mpya wa Ukrain Petro Poroshenko.

Pia wameonya kuwa hawatasita kuiwekea Urusi vikwazo zaidi iwapo itakataa kusaidia kurejesha uthabiti Ukrain.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa miaka 17 ambapo G7 inakutana bila Urusi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii