Biashara ya viungo vya binadamu Brazil

Image caption Makaburi ya umma Brazil

Viongozi wa mashitaka nchini Brazil , wanachunguza madai kuwa viungo vya miili vinatolewa kwa miili ya watu wasiojulikana na kuuzwa kwa ajili ya utafiti wa kimatibabu.

Viongozi wa mashitaka wameambia BBC kuwa viungo vinataolewa kwa miili ya watu waliofariki bila ya kufanyika juhudi za kuwatafuta jamaa zao watu hao ili kupata ruhusua kutoka kwao.

Hadi hivi karibuni, maiti zilizopatikana kando ya barabara au katika hospitali za umma huzikwa katika makaburi ya umma ikiwa hakuna aliyekuja kudai miili hiyo kwa muda wa masaa 72.

Hata hivyo moja ya shirika linalodaiwa kufanya uhalifu huo wa kuuza viungo vya miili ya watu wasiojulikana limekanusha madai hayo.

Image caption Familia kadhaa zinasema miili ya jaa wao inazikwa katika makaburi ya umma ilihali wanajulikana

Kuuza viungo vya miili ya watu ni kinyume na sheria ya Brazil.

Uchunguzi huu ulioanza mjini Sao Paulo, mwaka jana, ulianzishwa na polisi kutokana na madai ya familia kwamba maafisa wakuu hawakuwashauri kabla ya kuzika jamaa zao waliofariki katika makaburi ya umma ya Perus.

Baadaye mmoja wa walioshuhudia vitendo hivyo walifahamisha polisi kuwa viungo hutolewa kwa miili ya wafu na kutumiwa kwa utafiti wa kimatibabu bila idhini ya jamaa wa wafu.

Hata hivyo viongozi wa mashitaka wanasema kuwa hawana ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya biashara ya viungo vya binadamu.

Image caption Polisi wanasema kuwa bado wanaendelea na uchunguzi kubaini ukweli wa madai

Lakini uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa katika miaka 15 iliyopita, miili 3000 ilitolewa katika vyumba vya kuhifadhia maiti na kuzikwa katika makaburi ya umma , licha ya kwamba zilikuwa na stakabadhi za kuzitambulisha.

Shirika la SVO linaloendeshwa na walimu kutoka katika chuo kikuu cha Sao Paulo, linasema kuwa kwa kawaida wao hutumia miili tu ambayo imeshatambulishwa wanapotafuta viungo vya utafiti.

Walimu hao wanasema huwa hawatumii miili ambayo wenyewe hawajulikani.