Nyota wa Tennis mahakamani Afrika.K

Image caption Madai dhidi ya Hewwit yanasemekana kutokea wakati alipokuwa kocha wa watoto

Mchezaji bingwa wa zamani wa Tennis duniani, Bob Hewitt amefikishwa mahakamani nchini Afrika Kusini kwa kosa la ubakaji na kuwanyanyasa watoto kijinsia.

Hii ni kwa mujibu wa mawakili wake.

Hewitt, ambaye kesi yake itaanza Februari mwaka 2015, amekanusha mashitaka matatu dhidi yake.

Mashitaka hayo yanahusiana na kipindi alichokuwa kocha wa watoto nchini Afrika Kusini mwaka 1980.

Bwana Hewitt, mwenye umri wa miaka 74, alishinda mataji tisa ya Grand Slam kwa wachezaji wawili kila upande katika miaka ya sitini na sabini.

Mzaliwa wa Australia , nyota huyo wa zamani wa Tennis alifikishwa katika mahakama ya Boksburg mjini Johannesburg, kwa mara ya kwanza Ijumaa.

Wakili wake aliambia mahakama kwamba mtuhumiwa alielewa fika madai yote dhidi yake na kusema anayakana yote matatu, mawili ya ubakaji na moja la unyanyasaji.

Vyombo vya habari nchini humo vimesema kuwa bwana Hewitt alionekana mnyonge na kwamba hata alisaidiwa kutembea wakati alipokwenda mahakamani.