Rais wa Ukraine aapishwa rasmi

Image caption Rais mpya wa wa Ukraine Petro poroshenko

Rais mpya wa Ukraine ,tajiri Petro Poroshenko ameapishwa rasmi hii leo katika sherehe iliyofanyika katika bunge la taifa hilo mjini Kiev.

Katika hotuba yake ya kwanza mda mfupi tu baada ya kuapishwa Poroshenko amesema kuwa anataka kulirudisha taifa hilo katika hali yake ya asili ya Ulaya.

Amesema hataki vita wala kulipiza kisasi na kwamba ataanza kufanya kazi kupitia mpango wa amani utakaohakikisha kuwa watu wote wanalindwa licha ya matendo yao.

Amesema kuwa atafanya kazi ili kuhifadhi umoja wa taifa hilo na kwamba eneo la Crimea litasalia kuwa chini ya ardhi ya Ukraine.

Ameongezea kuwa atatia saini mkataba wa kuwaruhusu raia wa Ukraine kusafiri katika mataifa ya muungano wa ulaya bila vikwazo vyovyote.

Amesema kuwa hatua hiyo ndio ya kwanza ya kutaka Ukraine kuwa mwanachama kamili wa muungano wa Ulaya.