Mabaharia wa meli ya Malaysia waachiliwa

Mabaharia 11 wa meli moja ya Malaysia iliotekwa nyara na maharamia wa Somali wameachiliwa huru baada ya kuwa mateka kwa takriban miaka mitatu.

Mabaharia hao kutoka Kusini mwa bara Asia na Iran walikuwa wameabiri meli hiyo ya makasha MV Albedo wakati ilipotekwa nyara yapata kilomita 1500 kutoka pwani ya Somali.

Maelezo kuhusu vile walivyoachiliwa bado hayajatolewa,lakini afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa Nick Kay amesema kuwa wanasafirishwa hadi nchini Kenya kabla ya kurudishwa makwao.

Mabaharia saba wa meli hiyo waliwachiliwa miaka miwili iliopita baada ya kikombozi kulipwa.

Sita wengine wamefariki mmoja akipigwa risasi huku wengine wakifa maji baada ya kimbunga kikali kupiga meli hiyo mwaka uliopita.

Umoja wa mataifa unakadiria kwamba takriban watu 40 bado wanazuiliwa na maharamia wa kisomali .