Uwanja wa ndege washambuliwa Pakistani

Haki miliki ya picha AFP GETTY
Image caption Wanajeshi wa Pakistan wakiwa kwenye uwanja wa ndege wa Karachi kukabiliana na washambulizi.

Mapambano ya risasi yaliyodumu saa tano katika uwanja wa mji mkubwa zaidi nchini Pakistani ,Karachi yamewauwa watu 23 wakiwemo washambuliaji wote 10.

Washambuliaji hao waliokuwa na silaha nzito nzito waliingia sehemu ya majengo ya uwanja huo kupitia njia zinazotumiwa na ndege za mizigo au zile zinazotumiwa kuwapokea wageni wenye hadhi na sifa yaani V.I.Ps.

Walipenya usiku wa manane na kuanza kuwashambulia maafisa usalama kwa gruneti na kwa kuwafyatulia risasi.

Makamanda katika jeshi waliitwa kukabiliana na washambuliaji hao na milio ya risasi ilisikika hadi alfajiri wakati hali ilipodhibitiwa.

Haijabainika vyema ni akina nani hasa walioshambulia lakini yamewahi kufanyika mashambulio kama hayo hasa katika maeneo ya wanajeshi wa angani na wa majini ambapo wanamgambo wa Taliban walihusika.