Mhubiri mwingine auawa nchini Kenya

Image caption Marehemu Sheikh Mohammed Idris ameuawa na watu wasiojulikana

Hali ya ulinzi imeimarishwa mjini mombasa kufuatia kuuwawa kwa Muhubiri mmoja wa kiisilamu mapema leo asubuhi.

Ripoti zinasema muhubiri huyo ambaye ni mwenyekiti wa chama cha maimamu na wahubiri wa kiislamu, Sheikh Mohammed Idris, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa njiani kuelekea msikitini kwa sala ya asubuhi.

Kamishna mkuu wa jimbo la pwani mwa Kenya Mombasa, Marwa amesema uchunguzi unaendelea ili kubainmisha waliohusika na mauaji hayo na dhamira yao.

Kufikia sasa hakuna mshukiwa yeyote aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo. Mbarak hamisi ni muadhini katika msikiti wa manyatta ana aelezea kilichotokea.

Muhubiri huyo amezikwa leo alasiri chini ya ulinzi mkali wa polisi. Mauaji hayo ni mauaji ya hivi karibuni zaidi ya kiongozi mwingine wa kidini.

Ripoti zinasema kuwa muhubiri huyo alikuwa amepokea vitisho kutoka kwa vijana wenye itikadi kali za kidini na tayari alikuwa ameelezea hofu juu ya maisha yake kwa vyombo vya dola.

'Alipinga itikadi kali za kidini'

Image caption Vijana wa Mombasa wanasemekana kuanza kufuata itikadi kali za kidini zinazoenezwa na Al Shabaab

Sheikh Mohammed Idris, alikisiwa kuwa miongoni mwa wahubiri wa kiislamu ambao wanapinga itikadi kali za kidini.

Wahubiri kadhaa mashuhuri wenye itikadi kali nchini Kenya wameuawa katika hali ya kutatanisha miaka ya hivi karibuni.

Baadi yao walituhumiwa kuwachochea vijana kuwa na itakadi kali za kidini na pia kuwa na uhusiano wa karibu na kundi la wanamgambo la al-Shabaab nchini Somalia.

Hata hivyo wafuasi wa wahubiri hao waliouawa wameielekezea lawana serikali kwa kuwalenga viongozi wao na kutekeleza mauaji ya kidini kwa misingi ya kupambana na ugaidi. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametaja kifo chake kama pigo kubwa katika harakati za serikali za kupambana na siasa za itikadi kali.

Ubalozi wa Uingereza mjini Nairobi pia umelaani mauaji hayo ni kutaja kama pigo kubwa katika haraka za kupambana na ugaidi katika Pwani ya Kenya.

Afisa mmoja wa cha maimu ahmed Kassim amelaani mauaji hayo na kutaka serikali kuwahakikishia usalama wakati wanapoendelea na majuku yao.

Kabla ya kifo chake Sheikh Mohammed Idris, alikuwa ameitaka serikali kukabiliana na baadhi ya watu wenye itikadi kali za kidini ndani ya msikiti hali ambayo ilisababisha baadhi ya waumini kumuita msaliti.

Alikuwa mwenyekiti wa kamati ya msikiti mmoja maarufu ambao uongozi wake ulitwaliwa na vijana ambao wanapinga mahubiri yake ya wastani.