Serikali na waasi kumaliza mazungumzo

Haki miliki ya picha
Image caption Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Dkt Riek Machar

Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr na kiongozi wa waasi Riek wamekubaliana kufanya mazungumzo ya kubuni serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa.Mwenyekiti wa jumuiya ya ushirikiano wa kiserikali wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD, waziri mkuu wa Ethiopia Hailemarriam Desalegne, amesema kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kukomesha vita huko Sudan Kusini.

Baada ya mkutano wa zaidi ya saa nne katika ikulu ya waziri mkuu wa Ethiopia, mwenyeji wa mkutano huo Hailemarriam Desalegne alitangaza kuwa Kirr na mwenzake Machar wako radhi kushirikiana.

"Viongozi wa pande mbili, wamekubali kumaliza mazungumzo katika siku sitina zinazokuja, yatakayosababisha kuundwa kwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa", alisema Desalegne.

Ni kwa sababu hiyo vikao vitaanza Addis Ababa baina ya washirika wa Salva Kirr, Riek Machar na wale kutoka katika mashirika ya kijamii kujadili jinsi ya kuirejesha Sudan Kusini katika njia amani.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kukutana tangu watie mkataba wa kusitisha vita nchini Sudan Kusini.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Desalegne, amesema uamuzi huo umefikiwa kukomesha vita

Jitihada za IGAD

Shirika la IGAD ambalo limekuwa likiongoza juhudi za upatishi katika mzozo mzozo huo uliodumu kwa miezi saba, limeruhusu umoja wa mataifa kutuma vikosi vya usalama nchini Sudan kusini, kulinda amani kama inavyohitajika kutoa ulinzi kwa waangalizi nchini humo.

Ijapokuwa Machar na Kirr walikuwepo katika mkutano huo hakuna aliyezungumza.

Mbali na waziri mkuu wa Ethiopia, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alikuwa miongoni mwa walioendesha mkutano huo.

Tangu mapigano hayo yaanze maelfu ya watu wameuawa na zaidi ya milioni moja kupoteza makaazi yao.