Mashoga wapinga Urais wa Kutesa UN

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uganda, Sam Kutesa.

Uwezekano wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uganda, Sam Kutesa, kushinda cheo cha Urais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumeanzisha mjadala mkali nchini Uganda, huku wakereketwa wa haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda wakipinga asichaguliwe.

Ingawa Urais huo katika Umoja wa Mataifa hauna mamlaka makubwa lakini wakereketwa hao wanasema kuwa cheo hicho cha heshima hakipaswi kupewa Afisa wa cheo cha juu katika Serikali ya Uganda kwa sababu Taifa hilo la Afrika Mashariki lilipitisha sheria ambayo wanasema inawabagua wapenzi wa jinsia moja.

Hatua hiyo ya Uganda ilikosolewa na makundi mbalimbali duniani.

Maelfu ya wakereketwa hao wametia sahihi katika ombi kwenye mtandao wakisema kuwa kuchaguliwa kwa Bwana Kutesa kama Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni madharau kwa maadisi ya Umoja wa Mataifa.

Seneta wa New York, Kirsten Gillibrand pia itakuwa "hatua ya kusikitisha kumwona Waziri wa Mashauri ya Kigeni kutoka taifa lililopitisha sheria isiyo na haki, ya kudhulumu na ya kubagua kuwa kinara wa shirika hilo la kimataifa.."

Hapa alikuwa akigusia Sheria inayoharamisha mapenzi ya jinsia moja iliyopitishwa Februari ambayo inaruhusu watu wanaoshiriki mapenzi hayo kufungwa maisha gerezani.

Bwana Kusesa, mwanadiplomasia mkongwe mwenye umri wa miaka 65 alisema hivi majuzi kuwa "waafrika wengi wanachukia ushoga."

Urais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hauna mamlaka na hutolewa kwa mtu kutoka maeneo mbalimbali kila mwaka.

Mwaka huu ni zamu ya Afrika kumteua Rais huyo na Bwana Kutesa amekubaliwa na Bara lote bila kupingwa.