Wapiganaji waislamu wateka mikoa Iraq

Image caption Wapiganaji wa ISIS nchini Iraq wakijiandaa kwa mashambulio.

Wapiganaji wa Kiislamu wanadaiwa kuendelea na kuteka maeneo zaidi nchini Iraq, katika hatua ambayo Marekani imetaja kama ni tishio kwa eneo zima.

Polisi wa Iraq wanasema kwamba muungano wa makundi hayo - Islamic State of Iraq na Levant - ambao wanajiita kwa pamoja ISIS wameteka mikoa ya Kirkuk na Salehddin.

Inasemakana watu nusu milioni tayari wametoroka Mosul, eneo ambalo lilitekwa na wapiganaji hao jana. zaidi. Inadaiwa kuwa wapiganaji hao tayari wameteka mji mkuu wa pili kwa ukubwa nchini Iraq wa Mosul, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.

Wanajeshi na polisi wa wanadaiwa kuwa wametoroka baada ya makabiliano makali na wapiganaji hao wa kundi la Islamic State kutoka Iraq na Syria, wanaojulikana kama ISIS, likiwa ni kundi lililochipuka kutoka Al Qaida.

Wapiganaji wa ISIS wamekuwa wakisimamia shughuli za Mkoa wa Mosul kwa njia isiyo rasmi kwa miezi kadhaa sasa, ambapo wametoza kodi kwa bidhaa zote zinazoingia na kuondoka eneo hilo na wakati huohuo kupokea pesa za kutoa ulinzi kwa maafisa wa Serikali katika Mkoa huo.

Lakini hivi sasa, siku nne baada ya mapigano nje ya mijengo kadhaa muhimu katika eneo hilo inaonekana wazi sasa kuwa wameudhibiti mji wote wa Mosul, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq ulio na watu wanaozidi milioni mbili wakati kuna amani.

Image caption Mamilioni ya watu wameanza kuitoroka miji iliyotekwa na wapiganaji

Gavana wa mji huo, Atheel al-Nujeifi, alitangaza ombi kwa wanaume wote kujitolea kupambana na wapiganaji hao wa Kiislamu.

Maelfu ya watu wametoroka Mosul na kukimbilia eneo la karibu linalosimamiwa na Wakurdi.

Uwanja wa ndege hapo mjini, makao makuu ya kijeshi na taasisi zingine muhimu zimeshikiliwa na ISIS.

Inadaiwa kuwa vituo vingi vya polisi vimemeteketezwa na kituo cha televishemi hapo mjini kilionyesha moshi mkubwa ukipaa katikati mwa jiji huku mamia ya wafungwa wakionyesha kuwa wameachiliwa.

Shambulio hilo ni changamoto kubwa kwa Waziri Mkuu wa sasa Nouri al-Maliki.

Mnamo Januari wapiganaji wa ISIS na Wasunni wengine wasioridhika waliuteka mji wa Falluga ulio Magharibi mwa Baghdad, kitendo ambacho kilimshinda Bwa Maliki kupindua.