Vurugu kombe la dunia likikaribia kuanza

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano Brazil

Polisi katika mji wa Sao Paulo nchini Brazil wametumia gesi ya kutoa machozi kutawanya umati mdogo uliokuwa unaandamana kupinga kuandaliwa kwa kombe la dunia saa chache kabla ya kuanza kwa kinyang'anyiro hicho.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa polisi waliwarushia risasi za mipira waandamanaji.

Waandamanaji hao walisema kuwa walipanga kuusogea uwanja wa Corinthians Arena ambapo sherehe za ufunguzi zitafanyika kabla ya Brazil kucheza na Croatia.

Mtu mmoja alikamatwa huku mwandishi wa CNN akijeruhiwa.

Waandamanaji walisema kuwa walipanga maandamano hayo karibu na uwanja ambako kutafanyika sherehe za ufunguzi.

Maandamano zaidi yamepangwa kufanyika katika miji mingine nchini humo kupinga gharama ya maandalizi ya michuano hiyo.

Picha za Televisheni zimeonyesha polisi wa kupambana na ghasia wakitumia gesi ya kutoa machozi na risasi za mipira kuwatawanya karibu waandamanaji 50 karibu na kituo cha treni kuelekea katika uwanja wa Corinthians.

Waandamanaji hao walikuwa wakisema kwa sauti kuwa 'michuano hiyo haitafanyika'

Mwaka jana zaidi ya watu milioni moja walijiunga na maandamano kote nchini humo kutaka huduma bora zaidi za umma na pia kuangazia swala linalowakera la gharama ya juu ya maisha na pia kupinga gharama ya juu ya kuanda michuano hiyo.

Tangu hapo, maandamano mengine madogo ya kupinga kombe la dunia yamekuwa yakifanyika Brazil huku baadhi yakigeuka na kuwa ghasia.