Maliki awatia shime makamanda wake

Wanamgamo wa Ki-shia waliojitolea kwenda kupigana Haki miliki ya picha

Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki, amehutubia makamanda wake wa jeshi katika mji wa Samarra, kaskazini ya Baghdad - mpaka wa mapigano dhidi ya washambuliaji Waislamu ambao wameteka eneo kubwa la magharibi na kaskazini mwa nchi.

Alisema wanamgambo waliojitolea kupigana wanakusanyika mjini humo kuzuwia washambuliaji wasisonge mbele; na alisema Samarra ndipo panapoanza pambano dhidi ya washambuliaji.

Wanajeshi wa Iraq wakisaidiwa na wanamgambo wanaozidi kuongezeka, Wa-Shia na Wa-Kurd, wanajaribu kuyahami majimbo ya Salahaddin na Diyala, kaskazini ya mji mkuu.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq ametoa wito kuwa wanajeshi wa Iraq wasikithiri katika operesheni zao, wasije wakawadhuru raia.

Uingereza imetangaza kuwa itatoa dola milioni tano kwanza, kugharimia msaada wa dharura kwa maelfu ya wakimbizi.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani, anasema nchi yake iko tayari kushirikiana na Marekani kupigana na washambuliaji Waislamu nchini Iraq.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Rouhani alisema mataifa hayo mawili yanaweza kushirikiana kurejesha usalama nchini Iraq, iwapo Iran itaona kuwa Marekani inapambana na yale aliyoyaita makundi ya ugaidi, nchini Iraq na kwengineko.

Rais wa Iran amesema nchi yake bila ya shaka itaisaidia serikali ya Iraq ikiwa itaombwa.

Inaarifiwa kuwa jenerali mmoja wa Iran yuko mjini Baghdad ingawa Iran imekanusha kuwa wanajeshi wake wanashiriki vitani.