Misri kumwachilia mwanahabari wa Al Jazeera

Image caption Waandishi wengine wa Al Jazeera bado wanazuiliwa na serikali ya Misri

Kiongozi wa mashitaka ya umma wa Misri ameamuru kuachiliwa kwa mwanahabari wa Al-jazeera Abdullah Elshamy kwa misingi ya kiafya.

Bwana Elshamy amekuwa akigoma kula kwa takriban miezi 5 kulalamikia kukamatwa kwake bila kufunguliwa mashitaka.

Alikamatwa mwezi Agosti mwaka uliopita wakati polisi walitawanya maandamano yaliyokuwa yakifanywa na waandamanaji waliokuwa wakimuunga mkono rais Mohammed Morsi aliyeondolewa mamlakani.

Koti moja jijini Cairo lilikuwa limesema hapo awali kuwa lingetoa uamuzi wake juma lijalo kuhusiana na kesi iliyowakabili wanahabari wengine 3 wa Al-Jazeera waliokamatwa Disemba.

Image caption Wandishi ambao bado wanazuiliwa walidaiwa kuchochea ghasia Misri

Mwandishi wa habari wa zamani wa BBC Peter Greste na wenzake Mohamed Fahmy na Baher Mohamed wanashutumiwa kwa kusambaza habari za uwongo na kushirikiana na vuguvugu la kiisilamu Muslim Brotherhood ambalo linahusishwa na ugaidi.

Waendesha mashtaka wametaka korti kutoa hukumu kali angaa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa washukiwa, ambao walikana mashitaka.

Bwana Elshamy ambaye anaripotiwa kudhoofika kiafya alikuwa miongoni mwa watu 13 ambao mwendesha mashtaka mkuu aliamua kuwaachilia kwa misingi ya kiafya siku ya Jumatatu. 12 waliosalia ni waliokuwa wakiunga mkono kikundi hicho.

Familia yake bwana Elshamy iliiambia shirika la habari la AFP mwezi Mei kuwa alikuwa amepoteza kilo 40 tangu alipoanza kususia chakula.

“Ombi letu la kuachiliwa kwa Abdullah lilikubaliwa na mwendesha mashtaka mkuu,” alisema wakili wake, Shaaban Saeed siku ya Jumatatu. “Atatoka katika gereza la Torah pindi tutakapokamilisha utaratibu wa kuachiliwa kwake Jumanne asubuhi.”

Bwana Elshamy anafanyia kazi shirika la habari Al-Jazeera, idhaa ya Kiarabu.