Kwa nini Mpeketoni ilishambuliwa?

Saa nne unusu jioni Jumapili, Ufaransa ilikuwa inacheza dhidi ya Honduras katika mojawapo ya mechi za kombe la dunia.

Lakini mechi ilipokuwa inaendelea,katika eneo la Mpeketoni mauaji ya kinyama yalikuwa yakifanyika.

Ujumbe kutoka kwa afisa mmoja wa shirika la msalaba mwekundu ulikuwa na ishara zote za mashambulizi ya kigaidi sawa na kile ambacho wengi wamekuwa wakishuhudia katika mbinu ya mashambulizi inayotumika na Boko Haram nchini Nigeria.

''Milio mikubwa ya risasi inasisika katika eneo la Mpeketoni, katika jimbo la Lamu. Mashambulizi yamekuwa yakiendelea kwa saa moja sasa. Kituo cha petroli kimeteketezwa na hoteli kushambiliwa.Tunasubiri taarifa zaidi,'' alisema afisaa huyo wa shirika la Red Cross.

Usiku wa kuogofya wenye mashambulizi ambayo yalidumu kwa muda wa saa kumi. Walioshuhudia walisema waliona zaidi ya watu 50 wakiwa wamejihami vikali na kuanza kufanya msako ndani ya nyumba za watu.

Magari mawili yaliyokuwa yameibwa ndiyo yaliyotumika kuwabeba washambulizi hadi katika eneo la Mpeketoni umbali wa kilomita 40 kutoka ufuo wa bahari hindi.

Mashambulizi hayakuharakishwa. Washambuliaji walisemekana kuongea Kisomali na kiswahili huku wakibeba bendera ya Al Shabaab na kutamka 'Allahu Akbar'', yaani Mungu ni mkubwa.

'Kwa nini Mpeketoni? '

Eneo hilo ambalo halina ulinzi mkali bila shaka lilikuwa sehemu ya karibu sana kwa Al Shabaab kushambulia. Linakaribiana na Somalia. Kundi hilo halikusita kukikri kutekeleza mashambulizi hayo, saa 24 baadaye.

Walioshuhudia walisimulia visa vya kuogofya wakati washambuliaji walipokuwa wanaendesha mashambulizi nyumba hadi nyumba wakimuua kila mwanamume waliyemuona

Wanawake na watoto walisazwa. Mashambulizi yalifanya kwa masaa kadhaa kabla ya polisi kuchukua hatua.

Mfumo wa mashambulizi na ukubwa wa mashambulizi yenyewe umewaacha wengi wakiwa na maswali si haba. Kwa nini Mpeketoni? Na kwa nini wanaume pekee ndio waliouwa?

Al Shabaab walituhumiwa kwa mauaji ya wanawake na watoto katika shambulizi la awali dhidi ya jengo la kifahari la Westgate mwaka jana mjini Nairobi.

Mashambulizi ya kiholela ambayo pia yaliwalenga waisilamu, yaliwaghadhabisha wale ambao huunga mkono kundi hilo.

'Al Shabaab wabadili mbinu'

Al Shabaab sasa wameamua kubadili mbinu wanaotumia kushambulia kwa hofu ya kupoteza uungwaji mkono

Shambulizi la Mpeketoni, ilikuwa njia mojawapo ya kusafi sifa yao. Kuua wanaume na kuwasaza wanawake na watoto.

Mpeketoni ni eneo lenye rotuba nzuri ya kufanyia kilimo wala sio eneo ambalo ni kivutio kwa watalii. Maafisa wa usalama huenda walikutwa ghafla bila ya kujiandaa kukabiliana na shambulizi la aina yoyote.

Katika siku za nyuma, makundi ya kigaidi yamekuwa yakilenga miji mikubwa ya Kenya kwa mashambulizi lakini sasa inaonekana kuwa kundi hilo limeanza kubadili mbinu ya mashambulizi na kuanza kulenga vijiji.

Serikali ya Kenya imelaumu uchochezi wa kisiasa kwa mashambulizi hayo na kuwaonya wanasiasa dhidi ya kuchochea ghasia na matamshi ya chuki miongoni mwa wananchi.

Kuna mjadala mkali kuhusu nani aliyetekeleza mashambulizi hayo. Baadhi wanahisi kuwa licha ya kwamba Al Shabaab wamekiri kuyatekeleza, sio wao , serikali ya Kenya imesema wazi kuwa yalichochewa kisiasa.