Maiti yapatikana uwanja wa ndege Kenya

Image caption Polisi wanachunguza ikiwa mtoto huyo alianguka kutoka kwa ndege au la

Shughuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta zilisitishwa kwa muda Jumatano asubuhi baada ya maiti ya kijana mdogo kupatikana karibu na eneo la kurukia ndege

Mkuu wa kitengo cha Polisi katika uwanja huo, kamanda, Joseph ole Tito, amesema kuwa maiti hiyo ilipatikana katika sehemu ya kurukia ndege katika hali ambayo imewashangaza wengi.

Hata hivyo alisisitiza kuwa ndege zilizokuwa zinaingia uwanjani humo asubuhi na mapema hazikuathiriwa na tukio hilo.

Halmashauri ya huduma za ndege ilisema kuwa uwanja ulifungwa kwa dakika arobaini baada ya maafisa wa usalama kugundua maiti hiyo.

Kwa mujibu wa maafisa hao, hatua ya kufunga uwanja huo ilifanywa ili kuondoa mwili wa kijana huyo.

Ni ndege ya shirika la ndege la Uturuki tu ndiyo ililazimika kusalia angani kwa muda huku mwili wa kijana huyo ukiondolewa uwanjani.

Kijana huyo anaaminika kuwa na umri wa miaka 10 au12 na alikuwa na majeraha upande wa kushoto wa mwili wake.

''Mwili wake uliondolewa katika eneo hilo na kwamba uchunguzi unaendelea kufanywa,'' alisema bwana Tito.

Polisi wamesema watafanya uchunguzi kubaini ikiwa alianguka kutoka kwa gurudumu la ndege au mtoto huyo alifariki kutokana na sababu nyinginezo.

Pia miongoni mwa maswali yanayoulizwa ni vipi mwili wake ulipatikana katika uwanja wa ndege hasa katika njia ya kurukia ndege?

Visa vya watu kupanda kwenye magurudumu ya ndege kimagendo kwa lengo la kusafiri kwenda nchi nyingine vimekuwa vikiripotiwa hivi karibuni.