Hatma ya wakimbizi Kenya kujadiliwa

Image caption Waziri mkuu wa Somalia Abdiweli Sheikh Ahmed

Kenya na Somalia zinatarajiwa kurejelea mazungumzo kuhusu wakimbizi wa Somalia katika muda wa wiki mbili zijazo.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa Waziri mkuu wa Somalia Abdiweli Ahmed aliyezungumza na mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza katika ziara yake nchini Kenya Jumatano.

Mazungumzo hayo yalisimamishwa baada ya Somalia kulalamika kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa raia wa Somalia nchini Kenya, katika msako mkali uliofanywa kufuatia msururu wa mashambulio ya kundi la Al Shabab nchini humo.

Bwana Abdiweli anasema serikali yake imepata hakikisho kuwa haki zote za wakimbizi zitalindwa.

'Msako uliathiri wakimbizi Kenya'

Msako mkali uliotekelezwa na serikali ya Kenya dhidi ya wakimbizi wa Somalia uliibua mzozo mkubwa wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Aidha malumbano hayo yalisababisha mazungumzo kati ya Kenya na Somalia kuhusu wakimbizi hao kusimamishwa.

Bwana Abdiweli Sheikh Ahmed, alisema amepata hakikisho kutoka kwa Kenya kuwa juhudi zote za kuwahamisha wakimbizi zitazingatia sheria za kimataifa.

'Wengi walituhumu msako'

Mamia ya wakimbizi kutoka Somalia walikamatwa katika msako mkali na kuzuiliwa katika uwanja mmoja wa michezo jijini Nairobi.

Hata hivyo hatua hiyo ilikashifiwa vikali na serikali ya Somalia na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu.

Wakati huohuo, Sheikh Ahmed amesema serikali ya Kenya na Somalia zitaanza kushirikiana katika kubadilishana taarifa za kijasusi ili kukabiliana na kundi la Al Shabab.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kambi ya wakimbizi nchini Kenya

Waziri huyo mkuu anasema tayari Somalia imeanza kushuhudia manufaa ya vikosi vya AMISOM nchini humo, ambavyo hivi majuuzi vimekomboa miji tisa kutoka mikononi mwa wapiganaji wa AL Shabab.

Hata hivyo kundi hilo limeonekana kuendeleza mashambulizi makali nchini Somalia baada ya kutekeleza mashambulizi katika majengo ya bunge na ikulu ya Rais.

Aidha Kenya pia imeshuhudia ongezeko la mashambulizi yanayodaiwa kutekelezwa na wapiganaji hao wa Al Shabaab