Wandishi wa Al Jazeera wafungwa jela

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Greste na watuhumiwa wenzake wakiwa wanasubiri hukumu yao

Mahakama nchini Misri imewahukumu jela kifocngo cha kati ya miaka saba na kumi wandishi watatu wa habari wa shirika la habari la Al Jazeera waliokuwa wamezuiliwa kwa miezi sita nchini humo.

Walipatikana na hatia ya kueneza habari za kupotosha na kushirikiana na kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Muslim Brotherhood.

Mmoja wa wandishi hao ni Peter Greste, raia wa Australia na ambaye pia alikuwa mwandihi wa habari wa BBC wakati mmoja alipokea hukumu ya kifungo cha miaka saba.

Mwenzake Baher Mohamed alifungwa jela miaka kumi.

Watuhumiwa wengine kumi na moja waliohukumiwa bila ya wao kuwepo gerezani, walipokea vifungo vya miaka 10 kila mmoja.

Hukumu ilipotolewa, Greste kwa hasira aligonga mkono wake katika eneo ambako walikuwa wamezuiliwa huku mwenzake akibururwa kutoka mahakamani na walinzi wa gerezani.

Image caption Wandishi watatu wa Al Jazeera wamefungwa miaka 7 jela kwa kueneza habari za kupotosha

Familia za watuhumiwa nao wakaangua kilio. Kesi hii imelaaniwa sana kote duniani hasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na mashirika ya habari ya kimataifa.

Lakini nchini Misri, vyombo vya habari vilipeperusha habari hiyo kwa utofauti mkubwa.

Al Jazeera - ni shirika linaloonekana kuunga mkono vuguvugu haramu la Muslim Brotherhood na kwa mtanzamo huo , ni adui ya serikali.

Peter Greste ,ndiye alikuwa anaripoti matukio nchini Misri Disemba mwaka jana wakati wa harakati za mapinduzi.

Kisha yeye na wenzake wawili wakatuhumiwa kwa kusaidia vuguvugu la kigaidi na kutangaza taarifa za kupotosha dhidi ya serikali na maslahi ya taifa hilo.

Madai ambayo serikali ya Australia imekuwa ikikanusha vikali.

Serikali ya Australia ilitoa taarifa yake ikisema kuwa imeshtushwa sana na uamuzi wa mahakama katika kesi ya Peter Greste. Imeelezea kushangazwa sana na hukumu iliyotolewa. Serikali imesema haielewi kabisa matukio haya.

Shirika la Al Jazeera lenyewe limepinga hukumu iliyotolewa dhidi ya wandishi hao, Peter Greste, Mohamed Fahmy na Baher Mohamed likisema kuwa inakiuka sheria.