Wanawake zaidi watekwa nyara Nigeria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa Boko Haram wanataka kutawala eneo la Kaskazini mwa Nigera kwa kutumia sheria ya kiisilamu

Inaripotiwa kuwa wanawake pamoja na wasichana sitini walitekwa nyara Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wiki iliyopita.

Ripoti zilizotolewa mwishooni mwa wiki iliyopita zilisema kuwa ishirini kati yao walichukuliwa na kundi linaloaminika kuwa Boko Haram.

Wanawake hao inaarifiwa walitekwa nyara katika eneo la vijijini ambakop mawasiliano ni magumu sana , sababu ya kupata habari hizi kuchelewa.

Wanawake hao walitekwa wakati wa uvamizi uliofanywa katika vijiji vilivyo katika wilaya ya Damboa katika jimbo la Borno.

Watu wanaotoroka vijiji ambavyo vilishambuliwa, wanasema kuwa wanawake na wasichana sitini walitekwa nyara wiki jana.

Baadhi ya watoto waliotekwa ni wadogo sana wa umri. Moja ya vijiji vilivyoshambuliwa ni kile cha Kummabza kilicho katika eneo la Damboa katika jimbo la Borno.

BBC hata hivyo haijaweza kuthibitisha idadi kamili ya watu waliotekwa nyara. Hali hii imefanywa kuwa ngumu'kwani maafisa wa eneo hilo bado hawajatoa tamko lolote kuhusu kisa hiki labda kutokana na hofu juu ya maisha yao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Serikali ya Nigeria imekuwa ikishinikizwa kuwanusuru waliotekwa nyara eneo la Chibok

Sio jambo la kushangaza kwamba tangu kutekwa nyara kwa wasichana miambili wa shule kutoka Chibok , wanawake wengine wametekwa nyara

Vijiji vingi katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria, vinakumbwa na utovu wa usalama na wakati ambapo Boko Haram wanapofanya shambulizi,wao huchukua muda mrefu wakifanya uporaji na mauaji.

Mwishoni mwa wiki, idadi kubwa ya watu waliuawa karibu na eneo la Chibok.

Zaidi ya wasichana 200 wa shule walitekwa nyara eneo la Chibok mwezi Aprili.

Walitekwa nyara kutoka shule yao ya mabweni na wapiganaji wa Boko Haram.

Serikali ya Nigeria imekuwa chini ya shinikizo kali za kuitaka ifanye jitihada za kuwaokoa wasichana hao.