Obama na Putin washauriana vita Ukraine

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Obama na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin

Rais Obama amefanya mashauriano zaidi juu ya Ukraine na mwenzake wa Urusi, Rais Vladmir Putin.

Hii ni baada ya viongozi wa kundi la watu wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine kutangaza kuwa wataheshimu masharti ya usitishaji wa mapigano wa siku nne.

Katika taarifa Ikulu ya White House ilipongeza mpango wa amani ulioandaliwa na Rais mpya wa Ukraine, Petro Poroshenko.

Inadaiwa kuwa Rais Barack Obama alimwambia mwenzake wa Urusi kuwashinikiza wanaounga mkono kujitenga nchini Ukraine kufuata kikamilifu masharti ya mapatano ya kusitisha mapigano na pia kuhakikisha kuwa silaha hazivuki mpaka na kuingia Mashariki mwa Ukraine.

Utawala wa Obama unatilia shaka ahadi zilizotolewa na viongozi wa Urusi na wale wa makundi yanayotaka kujitenga nchini Ukraine na unasema kwamba vitendo vitakavyofanywa baada ya ahadi hizo ndivyo vitakavyokuwa msema kweli.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji wanaotetea kujitenga na Ukraine

Msemaji wa Idara ya Mashauri ya ndani ya Marekani alisema kuwa Marekani ina ushahidi kuwa Urusi inaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa kundi la watu wanaotaka kujitenga nchini Ukraine.

Miongoni mwa misaada inayotolewa na Urusi ni vifaru magari ya kuwabeba wanajeshi yasiyoweza kupenya risasi.

Hata hivyo kulingana na habari kutoka Urusi, katika mashauriano hayo ya simu Rais Putni alisema makundi yanayopigana nchini Urusi yanapaswa kufanya mashauriano ya ana kwa ana na kuwa jeshi la Ukraine linapaswa kusitisha shughuli zake Mashariki mwa taifa hilo.

Viongozi wa kundi linalotaka kujitenga Mashariki mwa nchi hiyo wamekubali kusitisha mapigano hadi tarehe 27 mwezi huu.

Tangazo hilo lilitolewa na kiongozi wa eneo lililojitangaza kuwa Jamhuri ya Watu wa Donetsk, Alexander Borodai, linalingana na lile lililotolewa na wanajeshi wa Serikali ya Ukraine mnamo Ijumaa.

Waasi hao walikubali kusitisha mapigano baada ya mashauriano ya awali yaliyofanywa kama hatua ya mwanzo inayotangulia mazungumzo ya amani na Rais mpya wa Ukraine, Petro Poroshenko.