21 Wafariki katika mlipuko Abuja

Image caption 21 Wafariki katika mlipuko Abuja

Zaidi ya watu 20 wameaga dunia na wengine 52 wakajeruhiwa vibaya katika mlipuko wa bomu uliotokea katikati ya mji Abuja Nigeria .

Walioshuhudia wanasema kuwa mlipuko mkubwa ulitokea katika maduka maarufu ya Banex plaza katika mtaa wa Wuse mjini Abuja.

Mwanahabari wa BBC aliyeko huko alisema kuwa alihesabu miili 12 ya watu walioaga dunia katika hospitali moja mjini humo.

Sehemu hiyo ilikuwa imejaa wanunuzi wakati wa mlipuko huo.

Sauti ya mlipuko huo ulisikika mbali sana na eneo la tukio hilo.

Moshi mkubwa ulionekana juu ya mijengo iliyoko katika sehemu hiyo.

Magari mengi yaliyokuwa yameegeshwa nje ya duka hilo yaliteketezwa na vioo vingi vikavunjwa.

Image caption 21 Wafariki katika mlipuko Abuja

Haijulikani ni watu wangapi walijeruhiwa au kuuwawa, lakini wanaotoa huduma za dharura wamewapeleka watu wengi katika hospitali za karibu.

Jiji la Abuja limekuwa likilengwa kwa mashambulizi ya bomu katika miezi ya hivi karibuni na wapiganaji wa kundi la kiislamu wa Boko Haram.

Bomu moja lililokuwa limetegwa kwenye gari liliwauwa watu wasiopungua 15 mwezi Mei .

Shambulizi lingine katika kituo cha mabasi mwezi mmoja uliotangulia liliuwa watu wasiopungua 75, mashambulizi yote yakitekelezwa katika vitongoji vya jiji la Abuja.

Polisi wanasema kuwa tayari wamemtia mbaroni mshukiwa mmoja .

Hadi kufikia sasa hakuna kundi lililodai kutekeleza shambulizi hilo ijapokuwa macho ya wengi yanaelekezea lawama kwa kundi la wapiganaji wa kislamu wa Boko Haram ambao tayari wametekeleza mashambulizi kadha katika mji huo wa Abuja.