CAR:Usalama wazidi kuzorota yasema U.N

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jamhuri ya Afrika ya kati

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika nchi ya Jamhuri ya Africa ya Kati, Generali Babacar Gaye amesema kuwa usalama umezorota katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita na kuwa nchi hiyo inaweza kuathirika vibaya kutokana na hali hiyo.

Generali Gaye aliliambia baraza la usalama kuwa nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na mashambulizi hatari na uasi wa wanamgambo wa kiislamu na wakristo.

Zaidi ya watu 50 wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi katika siku chache zilizopita.

Afisa huyo wa umoja wa mataifa alitoa habari za kuhuzunisha kuhusu yanayofanyika katika nchi hiyo, mbele ya baraza la usalama.

"Takriban watu 20,000 wamezuiliwa katika maeneo machache", Generali Babacar Gaye alisema .

"wakiondoka, wanaweza kushambuliwa kabla hawajafika kwenye usalama".

Mji mkuu, Bangui, kwa sasa hauna idadi ile yake ya waislamu walio wachache kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa kikristo.

Waliobakia, wamezingirwa na watu waliojihami kwa silaha ambao wanawazuia kuondoka na pia kukata usambazaji wa vyakula na dawa.

Wanaojaribu kuwasaidia kupitia kusambaza huduma zozote zile, pia wanalengwa na wanamgambo hao.

Generali Gaye alisema kuwa ulinzi na usalama unahitajika eneo hilo.