70,000 kurejea kazini Afrika Kusini

Image caption Kiwanda cha dhahabu nyeupe Afrika Kusini

Maelfu ya wafanyakazi katika machimbo ya dhahabu nyeupe nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kazini hii leo Jumatano baada ya mgomo wa miezi mitano ambao umeathiri uchumi wa nchi hiyo.

Chama cha wafanyakazi hao cha AMCU kilitia sahihi mapatano mbalimbali na kampuni za Lonmin, Impala na Anglo American hiyo yana.

Wafanyakazi hao hawakupata mshahara waliotarajia wa Rand za Afrika Kusini 12,500 (zaidi ya Dola 1,000) lakini walikubali mkataba wa miaka mitatu ambapo wataendelea kuongezwa mshahara, penisheni, malipo ya nyumba na bima ya Afya.

Wafanyakazi zaidi ya 70,000 watafika kazini katika machimbo hayo ya dhahabu nyeupe hii leo lakini ni dhahiri kuwa itachukua miezi kadhaa kabla ya uzalishaji wa madini hayo kufikia hali yake ya kawaida.

Mkataba huo wa miaka mitatu uliotiwa sahihi pamoja na kampuni za Lonmin, Impala Platinum na American Platinum imemaliza mgomo mrefu zaidi kuwahi kutokea nchini Afrika Kusini na ambao umegharimu taifa pesa nyingi sana.

Wazalishaji wa dhahabu nyeupe walipata hasara ya Dola Bilioni 2 na wafanyakazi hao wakapoteza mishahara ya Dola Bilioni moja tangu mgomo huo uanze Januari mwaka huu.

Mgomo huo mkubwa pia ulivuruga uchumi wa taifa.

Chama cha wafanyakazi cha AMCU kinachowakilisha wengi wa wafanyakazi katika sekta ya dhahabu nyeupe kinasema kuwa ingawa mgomo ulikuwa chungu lakini matokeo yake ni matamu.

Chama cha AMCU kiliandaa mgomo wa Agosti 2012 ambapo wafanyakazi 34 walipigwa risasi na kuauwa na polisi katika machimbo ya Marikana.