Facebook yapinga kesi kuhusu data

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Facebook inasema mahakama ilikiuka katiba

Mtandano wa kijamii wa Facebook umekata rufaa dhidi ya amri ya mahakama ambapo ilitakiwa kuwasilisha data ya watu 400 waliouhusika na visa vya kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Mtandao huo wa kijamii ulisema kuwa ombi hilo la mahakama lilihusisha idadi kubwa ya majina ya watu kuwahi kuombwa na shirika la kiserikali kutoka kwa mtandao huo

Picha na ujumbe wa faragha pamoja na taarifa nyinginezo kuhusu watu hao ziliwasilishwa kwenye mahakama mwaka jana, lakini mahakama ilitoa tangazo hili wiki hii.

Uamuzi wa mahakama ulitaja Facebook kama mhifadhi wa data za kidijitali.

Jaji wa kesi hiyo alisema maana ya kuwa mhifadhi ni kwamba Facebook inapaswa kutii agizo la mahakama la kutaka kufanysa msako.

Kesi halisi ilichunguza visa vya watu kadhaa kudai malipo kutoka kwa mfuko wa taifa kwa watu wenye ulemavu Marekani.

Lakini akaunti zao za Facebook zilionyesha wakiwa hawana ulemavu wowote.

Mtandao huo ulilazimishwa kuwasilisha taarifa kuhusu akaunti za watu 381 ambazo mahakama ilisema zilikuwa na ushahidi kuonyesha watu hao walifanya uhalifu.

Baada ya ombi lao la rufaa kupinga agizo hilo kukataliwa, Facebook ilitii amri ya mahakama na kuwasilisha taarifa hizo ingawa ilisisitiza kuwa agizo hilo lilikiuka katiba ya Marekani ambayo inazuia msako wowote usio na msingi.

Kesi hiyo imekuwa ikisikilizwa faraghani lakini tangu Facebook kukata rufaa jaji wa kesi hiyo aliamua kuendesha kesi hiyo hadharani.