Mlipuko waua watu 10 nchini Nigeria

Takriban watu 10 wameuawa na wengine 14 kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea katika mji wa Bauchi Kaskazini mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa polisi, shambulizi hilo lililoripotiwa Ijumaa jioni lilitokea katika jengo linalojulikana kutumiwa kwa shughuli za ukahaba.

Kiini cha mlipuko hakijulikani ingawa wapiganaji wa Boko Haram wamewahi kushambulia mji wa Bauchi.

Mlipuko huo pia umetokea siku mbili tu baada ya shambulizi mjini Abuja kuwaua watu 22.

Takriban watu 10,000 wanakisiwa kuuawa na kundi la Boko Haram tangu kuanza harakati zao mmwaka 2009.

Wapiganaji hao hulenga maeneo ambayo wanayaona kuwa hayambatani na matakwa ya dini ya kiisilamu kama vile baa, makanisa na shule ambazo hutoa mafunzo ya kimagharibi.

Kundi la Boko Haram, limezua wasiwasi kimataifa hasa tangu lilipowateka nyara zaidi ya wasichana 200 katika eneo la Chibok mwezi Aprili.