Wagonjwa wa Ebola wasakwa Sierra Leone

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Madaktari wa kukabiliana na Ugonjwa wa ebola

Sierra Leone imeonya kuwa ni uhalifu mkubwa kwa mtu yeyote kuwapatia maficho watu wanaougua ugonjwa wa ebola.

Wizara ya afya imesema kuwa wagonjwa kadhaa wametoroka katika hospitali katika wilaya ya Kenema,ambayo ndio eneo la kwanza la kuzuka ugonjwa huo.

Shirika la afya Duniani WHO limetaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa ebola katika mataifa ya Magharibi ambao umewaua takriban watu 400.Ni ugonjwa wenye idadi kuu ya visa,vifo na ueneaji.

kumekuwa na visa 600 vya ugonjwa huo nchini Guinea ambapo mkurupuko huo ulianza miezi minne iliopita pamoja na mataifa jirani ya Sierra Leone na Liberia.

Asilimia 60 ya raia walioambukizwa na virusi vya ugonjwa huo wamepoteza maisha yao.

Haki miliki ya picha
Image caption Harakati za kuthibiti usambaaji wa ugonjwa wa ebola zaendelea

Shirika la afya duniani linasema kuwa nchini Sierra Leone pekee kumekuwa na vifo 46 kati ya watu 176 walioambukizwa ugonjwa huo.

WHO tayari imewatuma wataalam 150 katika eneo hilo ili kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Hatahivyo imeonya kwamba kuna uwezekano wa ugonjwa huo kusambaa hadi mataifa mengine.

Daktari Shek Moar Khan ambaye anawahudumia wagonjwa wa ebola katika hospitali kuu ya kanema amesema kuwa maafisa wake walikabiliwa na pingamizi wakati walipojaribu kuwaelezea wakaazi kuhusu ugonjwa huo.

Wafanyikazi wa idara ya afya nchini humo wamekuwa wakijaribu kuwaelezea raia katika maeneo ambayo yameathirika kwamba ''ugonjwa huo si wa siri na kwamba ni ugonjwa ambao unaweza kuambukizwa, na iwapo wangeweza kusikiza ushauri wetu basi tungepunguza usambazaji wa ugonjwa huo'',alisema.

Siku ya ijumaa shirika hilo la afya liliyaambia mataifa ya afrika magharibi kama vile Ivory Coast,Mali,Senegal na Guinea Bissau kujiandaa kwa wageni walio na maambukizi ya ugonjwa huo.