Mshukiwa wa Mpeketoni mahakamani

Image caption Dyana anasema kuwa alitekwa nyara na gari lake kuchukuliwa na washambuliaji

Mshukiwa mmoja aliyekamatwa na polisi kuhusiana na mauaji yaliyotokea Mpeketoni Pwani ya Kenya, alifikishwa mahakamani leo na kufunguliwa mashitaka ya mauaji ya zaidi ya watu kumi.

Mshukiwa huyo Dyana Salim Suleiman, amekanusha mashitaka hayo.

Dyana alijitetea kwa kusema kuwa gari lake lilitekwa nyara na kutumiwa kwa mashamulizi yaliyofanyika mjini Mpeketoni na kwamba alipigwa na kujeruhiwa vibaya huku akiachwa hali mahututi.

Mshukiwa huyo pamoja na wengine walifikishwa mahakamani Juni 23 ingawa hawakufunguliwa mashitaka wakati huo.

Wendesha mashitaka waliomba mda zaidi kukamilisha uchunguzi.

Zaidi ya watu sitini waliuawa mjini Mpeketoni katika mashambulizi ambayo yalizua malumbano nchini Kenya huku serikali ikidai yalichochewa kisiasa wakati kundi la Al Shabaab lilikiri kuwa ndilo lililotekeleza mashambulizi hayo.

Mali ya watu iliharibiwa katika mashambulizi hayo yaliyokuwa makubwa tangu kutokea mashambulizi dhidi ya jengo la Westgate mwaka jana.

Wakili wa Suleiman ameomba mahakama kumwachilia kwa dhamana akisema kuwa anaugua kisukari na kwamba kutamzuia kumeza dawa zake.