Magunia ya Kokeni yagunduliwa Ureno

Haki miliki ya picha spl
Image caption Kokeni hiyo ilifungwa ndani ya visanduku katika maduka ya jumla Ureno

Takriban magunia 200 ya kokeni yamepatikana yakiuzwa ndani ya visanduku katika maduka mbalimbali ya jumla nchini humo.

Polisi wanaamini kuwa kutambuliwa kwa mihadarati hiyo iliyoingizwa nchini humo kiharamu na walanguzi kutawasaidia kuwafuatilia waliohusika katika lile kinachodhaniwa kuwa kundi linalotekeleza operesheni yake kati ya Colombia na Ulaya.

Mnunuzi mmoja aliyekuwa akitafuta matunda katika sehemu ya duka moja la kijumla nchini Ureno alishtuka alipogundua kifuko kidogo cha kokeni ndani ya chane ya ndizi.

Kwa mujibu wa polisi, zaidi ya kilogramu 237 ya kokeni - iliyowekwa katika vifuko 198 tofauti, imepatikana katika visanduku katika maduka ya jumla sehemu mbalimbali kaskazini mwa taifa hilo.

Mihadarati hiyo iliingizwa pamoja na ndizi kutoka Colombia.

Walanguzi hao walisahau kuitoa mihadarati hiyo kutoka kwa vijisanduku hivyo vya ndizi.

Maafisa wa polisi Ureno, Uhispania na Marekani kusini kwa sasa wanafanya kazi pamoja kujaribu kuwakamata wanaojihusisha na kundi hilo linalotuhumiwa kuwa la ulanguzi.