Bomu laua wanne nje ya Bunge Somalia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wabunge wa Somalia

Bomu lililotegwa kwenye gari limelipuka na kuua watu wanne karibu na Bunge la Somalia, maafisa wa Polisi wamesema.

Habari zanasema bomu hilo lilipiga nje ya lango kuu la kuingia katika majengo ya Bunge la Somalia baada ya askari kumrushia risasi mtu ayedaiwa kulipua bomu hilo.

Taarifa zilizonukuliwa kutoka kundi la kigaidi la Al Shabaab zinasema wapiganaji hao walifanya shambulio la kujitoa sadaka.

Mlipuko mwingine uliofanywa na waasi hao katika majengo ya bunge mwezi Mei uliuua watu 10.

Kundi la Al shabaab lilipoteza udhibithi katika mji mkuu wa Mogadishu tangu mwaka 2011 na tangu wakati huo limekuwa likiendesha mashambulizi ya mabomu na kufanya mauaji.

Mapema wiki hii Mbunge maarufu Ahmed Mohamud Hayd, aliuawa kwa kupigwa risasi katika mji huo, katika shambulio linalodaiwa kufanywa na Al Shabaab.