Upinzani washinikiza serikali Kenya

Haki miliki ya picha other
Image caption Odinga ataambatana na washirika wake akiwemo makamu wa zamani wa Rais Kalonzo Musyoka

Usalama umeimarishwa nchini Kenya huku upinzani ukijiandaa kwa mkutano mkubwa wa kisiasa ambao wameutaja kama kumbukumbu kwa mkutano na harakati za Saba Saba.

Mkutano huu umeandaliwa na kiongozi wa upinzani CORD Raila Odinga ambaye pia alikuwa waziri mkuu wa zamani na washirika wake.

Polisi wameanza doria katika Bustani ya Uhuru Park ambako mkutano huo utafanyika pamoja na maeneo mengine ya mji mkuu Nairobi.

Walianza kushika doria asubuhi na mapema wakiwa na Mbwa wa usalama.

Muungano wa CORD unatarajia mkutano huo kuwa mkubwa kuliko yote iliyowahi kufanyika nchini humo na kuongeza kuwa utalenga kushauriana na wakenya kuhusu hali ya nchi hiyo.

Pia wanasema kuwa lazima serikali ikubali kufanya mazungumzo nao ili kutafuta suluhu kwa matatizo yanayoikumba nchi hiyo ikiwemo kuzorota kwa usalama , uchumi, ukosefu wa ajira na mfumko wa bei.

Mkutano wenyewe unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa ingawa duru kutoka kwa chama cha CORD zinasema haijulikani mkutano huo utakapomalizika wakati gani.

Raila anatarajiwa kutoa hotuba na mapendekezo yake kwa serikali ambayo itayawasilisha baadaye.