Sudan Kusini yaadhimisha miaka 3

Haki miliki ya picha Xinhua
Image caption Baada ya miaka 3 ya kujitawala Sudan Kusini imesemekana kuwa nchi iliyoporomoka

Maelfu ya wananchi nchini Sudan Kusini wamejitokeza kushuhudia gwaride la kijeshi katika sherehe za kuadhimisha miaka mitatu tangu kujipatia uhuru.

Barabara za mji mkuu Juba, zimerembeshwa na mabango yenye kauli 'One People, One Nation'.

Ulinzi umedhibitiwa na duru zinasema kuwa kulikuwa na hali ya wasiwasi katika miezi saba ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya wafuasi wa Rais Kiir na aliekuwa makamu wake Riek Machar.

Takriban watu elfu kumi waliuawa katika vita hivyo, na wengine zaidi ya milioni moja kuachwa bila makao.

Mashirika ya misaada yameonya kuwa ukame unaotarajiwa nchini humo unaweza tu kuzuiwa ikiwa msaada zaidi wa chakula unaweza kupelekwa nchini humo.

'Mwiba wa kujidunga'

Image caption Bwana Ban anawataka viongozi wa Sudan Kusini kulela amani

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amedai kuwa ghasia za Sudan kusini ambazo zimesababisha maafa ya watu wengi ni mwiba wa kujidunga, huku akielekeza lawama kwa viongozi nchini humo na kuwataka wamalize ghasia hizo na kurejelea mazungumzo mara moja

Aidha, bwana Ban Ki-moon alisisitiza kuwa ni jukumu la rais Salva Kiir na Riek Machar kutumia uwezo walio nao kusitisha vita.

Ghasia hizo zilianza nchini humo baada ya rais Salva Kiir, ambaye ni m-Dinka, kudai kuwa aliyekuwa naibu wa rais Riek Machar alijaribu kupindua serikali.

Madai hayo yalisababisha vita baina ya makabila na juhudi za kurejesha amani hazikufua dafu.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, hapo jana bwana Ban Ki-moon akiwa nchini Sudan kusini alisema kuwa matumaini ya watu ya kuwepo kwa amani yamedidimia kwa sababu ya ghasia ambazo zimedunisha hali ya maisha na kusababisha njaa, magonjwa na ukosefu wa usalama nchini humo.

Image caption Kiir analaumiwa na jamii ya kimataifa kwa kukosa kuleta utulivu nchini humo

Msemaji wa bwana Ban Ki-moon alionya kuwa zaidi ya watu milioni moja nuka tatu wamehama makwao na iwapo msaada hautatolewa na watu kushirikiana, huenda ma-elfu ya watu wakaathiriwa na njaa miezi ijayo.

Mjumbe wa Umoja wa mataifa Hilde Johnson akiwa Juba aliarifu wanahabari kuwa Sudan kusini imerudishwa miongo mingi nyuma kwa sababu ya ukosefu wa amani. Hilde pia alisema kuwa utengano uliopo baina ya jamii hizo unakera mno na uhasama umekithiri inapolinganishwa na hapo awali na kwenye historia nzima ya Sudan kusini.

Kulingana na umoja wa mataifa, wanachi wa South Sudan wanaposherehekea miaka mitatu tangu kuzaliwa kwa nchi yao, wanachoona ni nchi iliyo katika hatari ya usalama na isiyo na matumaini ya kufuzu.