Wakurd wazozana na Maliki

Massoud Barzani, kiongozi wa Iraq Kurdistan Haki miliki ya picha

Ugomvi wa kisiasa baina ya jimbo la Iraq la Kurdistan na eneo lilobaki la Iraq, umezidi kuwa mkali.

Waziri wa Mashauri ya nchi za Nje wa Iraq, Hoshyar Zebari, mwanasiasa maarufu kabisa wa Kikurd katika serikali ya Iraq, ameiambia BBC kwamba Waziri Mkuu Nouri Al Maliki lazima aombe msamaha na abadilishe kauli yake kuhusu Kurdistan.

Alisema iwapo Bwana al Maliki hatafanya hivyo, basi Wakurd wataona tabu sana kufanya kazi naye.

Bwana Maliki hapo awali aliwashutumu wakuu wa Kurdistan kuwa wanawapa hifadhi wale aliowaita magaidi.

Kutokana na hayo, waziri wa mashauri ya nchi za nje pamoja na mawaziri wengine wa Kikurd waliacha kushiriki katika serikali.

Ugomvi hasa ulianza mwezi uliopita pale kiongozi wa Kikurd, Massoud Barzani aliposema kuwa anajitayarisha kwa kura ya maoni kuhusu uhuru wa Kurdistan.

Na Ijumaa ugomvi ulizidi pale Wakurd walipodhibiti visima viwili vya mafuta karibu na mji wa Kirkuk wenye utata.