Afghanistan:Kura kuhesabiwa upya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption John kerry kushoto akiwaangalia wagombea wa urasi Ashraf Ghani katikati na Abdulla Abdulla wakisalimiana.

Maafisa wa uchaguzi nchini Afghanistan wanajiandaa kuhesabu kura zote millioni nane zilizopigwa katika uchaguzi wa urais wa awamu ya pili.

Ni miongoni mwa makubaliano yalioafikiwa na waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry ili kumaliza mgogoro wa kisiasa kati ya Wagombea wawili Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah kufuatia madai ya udanganyifu katika shughuli hiyo.

Bwana Kerry amesema kuwa wagombea wote Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah wamekubaliana kufanyika kwa ukaguzi huo ambao utafanyika mjini kabul.

Masanduku ya kupiga kura kutoka mikoani yatasafirishwa hadi katika mji mkuu na vikosi vinavyoongozwa na NATO na kulindwa na vikosi vya kimataifa pamoja na wanajeshi wa Afghanistan.

Ukaguzi huo unalenga kutatua mgogoro huo wa kisiasa wakati ambapo wanajeshi wa Marekani wanaondoka nchini humo.

Vilevile utatoa fursa kwa mshindi kubuni serikali ya umoja wa kitaifa.