Malala azuru Nigeria kuwaenzi waliotekwa

Haki miliki ya picha PA
Image caption Malala Yousafzai akitoa hotuba yake.

Malala Yousafzai ambaye alipigwa risasi kwenye kichwa na wanamgambo wa Taliban nchini Pakistan miaka miwii iliopita anazuru mji mkuu wa Abuja nchini Nigeria ili kuendeleza kampeni yake ya elimu bora miongoni mwa wasichana na wanawake.

Aliwasili mjini humo akisheherekea mwaka wa 17 wa kuzaliwa kwake miezi mitatu baada ya zaidi ya wasichana 200 wa Nigeria kutekwa nyara na kundi la Boko Haram.

Katika taarifa yake, amesema kuwa ziara yake nchini humo ni kuwaenzi wasichana hao ambao walijitolea kupata elimu.

Malala alipigwa risasi kwa kuwa alikuwa anaongoza kampeni ya wasichana kupata elimu nchini Pakistan na baada ya kupona kwake nchini Uingereza aliapa kuendelea kampeni hiyo.

Ni nusu ya wasichana waliokuwa kati ya umri wa miaka sita na kumi na moja ambao huenda shule nchini Nigeria,licha ya kutajwa kama uchumi mkubwa barani Afrika.