Pistorius ajikuta pabaya klabuni

  • 15 Julai 2014

Mwanariadha wa Afrika Kusini anayekabiliwa na kesi ya mauaji, Oscar Pistorius, amedaiwa kuhusika katika malumbano ndani ya klabu moja nyakati za usiku mwishoni mwa wiki.

Mwanariadha huyo alikuwa katika klabu moja alipojikuta katika hali ya majibizano makali na mfanyabiashara mmoja aliyekuwa amemuuliza kuhusu kesi anayokabiliwa nayo.

Mfanyabiashara huyo Jared Mortimer anayedaiwa kumshambulia Oscar kwa maneno akimuuliza kuhusu kesi yake, anasema kuwa Pistorius alikuwa mlevi chakari wakati wa majibizano hayo.

Sarakasi hiyo ilitokea katika klabu ya kifahari mjini Sandton kufuatia madai kuwa Pistorius aliwatusi marafiki wa Jared Mortimer pamoja na kuitusi familia ya Rais wa Afrika Kusini Jaocb Zuma.

Madai haya ni kwa mujibu wa jarida la The Star.

"Nilichukizwa sana na matusi aliyoyatoa Pistorius kwa sababu nina uhusiano wa karibu sana na familia ya Zuma, '' alisema bwana Mortimer.

Bwana Mortimer aliongeza kuwa mwanariadha huyo alikuwa mlevi chakari na alianza kumsota kidole kifuani wakati walipokuwa wakiongea.

Mfanyabaishara huyo alisema alimsukuma mwanariadha huyo ambaye alianguka chini.

Walinzi katika klabu hiyo, walimsaidia Pistorius kusimama ingawa waliamrishwa kumpeleka nje ya klabu baada ya kuanza kumtusi mwanamume mwingine.

Msemaji wa familia ya Pistorius Anneliese Burgess, amekanusha madai ya Mortimer.

Pistorius anakabiliwa na kesi ya mauaji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp yaliyotokea mwaka jana akisema kuwa alimuua kwa bahati mbaya akidhani alikuwa jambazi aliyekuwa amevamia nyumba yao.

Kesi dhidi ya Pistorius iliahiirishwa wiki jana tayari kwa kauli ya mwisho kutoka kwa upande wa utetezi na wa mashitaka kabla ya uamuzi kutolewa.