Boko Haram wafanya mashambulizi tena

Haki miliki ya picha AFP

Watu kadhaa katika mji wa Dille, Kaskazini mashariki mwa Nigeria, wameuawa, na wengine kutorokea vijiji jirani baada ya kushambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram.

Aidha, nyumba kadhaa zilichomwa katika shambulizi hilo lililotekelezwa siku ya Jumatatu

Inasemekana kuwa raia walidhani kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na wanajeshi ili kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram bali sivyo.

Anavyoripoti Raliya Zubairu kutoka Abuja, viongozi nchini Nigeria wamedhibitisha shambulizi hilo, lakini hawajatoa usemi ni watu wangapi waliuawa.

Hata hivyo wanapeleleza madai ya raia kuwa walishambuliwa na ndege za wanajeshi.

Shahidi aliyezungumza na BBC alisema watu 25 waliuwawa, huku wanamgambo 20 wakiuawa na wakaazi wanaoshika doria katika eneo hilo.

Hayo yakijiri, wanaharakati wa haki za kibinadamu wametoa ripoti hii leo inayosema kuwa takriban watu elfu mbili wameuwawa na wanajeshi tangu mwanzoni mwa huu mwaka.