Adai ardhi kwa ufalme wake Afrika

Haki miliki ya picha BBC World Service

Mwanamme mmoja kutoka Marekani amedai umiliki wa kipande kidogo cha ardhi barani Afrika kama ufalme wake kwa sababu bintiye anataka kuwa binti mfalme.

Jeremy Heaton aliambia BBC kuwa amesafiri kutoka Virginia nchini Marekani na bendera yake kutangaza eneo hilo kwa Ufalme wa 'Sudan Kaskazini.'

Eneo hilo ni jangwa la mraba wa maili 800 lililo kati ya Misri na Sudan, na halijamilikiwa na nchi yoyote.

Alisema kuwa ameandikisha rasmi maombi kwa nchi hizo mbili, japo bado hajapa jibu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption 'Princess Emily' huvalia tiara kila mahali anapokwenda kuashiria kuwa yeye ni mwanamfalme

Bwana Heaton aliarifu BBC kuwa bintiye, Emily, aliuliza kwa sauti isiyo ya mzaha ‘iwapo siku moja angekuwa binti mfalme.’

“Kama babake, nilitambua kuwa ombi lake halikuwa mzaha, ” Heaton alisema.

“Nilitafiti vipande vya ardhi visivyomilikiwa na nikabahatika kuvigundua.”

Ili kuadhimisha miaka misaba tangu kuzaliwa kwa bintiye, Heaton alisafiri kwenda panapofahamika na wenyeji kama ‘Bir Tawil’ ili kutimiza ombi la Emily.

Heaton ambaye ana watoto watatu alisema kuwa angefanya lolote ili kudhibitishia wanawe kuwa anaweza kuenda “kokote kwa ajili yao.”

Tarehe 16, mwezi Juni, Heaton aliwasili jangwani na kuweka bendera iliyochorwa na bintiye, na kusisitiza madai yake ni halali.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Alidai kuwa kwa miaka mingi nchi kadhaa, ikiwemo Marekani, zilidai umiliki wa ardhi kwa kuweka bendera kwenye ardhi hiyo. Sasa bwana Heaton anasema atajaribu kuomba usaidizi kutoka kwa Umoja wa Afrika (AU).

Mzozo wa mipaka kati ya nchi ya Sudan na Misri unaashiria kuwa jangwa hilo ni kati ya vipande vya mwisho duniani visivyomilikiwa

Tofauti, anavyosema, ni kuwa aghalabu vita huzuka ili kupata umiliki huo, bali kwa kesi yake, “kuanzisha nchi hiyo ni ishara ya mapenzi yake kwa bintiye.”

Hata kama hakuna uwezekano kuwa Jeremy Heaton atakuwa mfalme wa nchi hiyo mpya ya Sudan kaskazini, ana mipango atakavyoendeleza “nchi hiyo.”

Binti mfalme Emily, aitwavyo sasa na familia yake, ametoa amri ardhi yake mpya iwe kituo cha ukulima. Sasa anavalia nguo za kimalkia na taji yake ya kifalme popote aendapo na anasema “inampendeza” kuwa binti wa mfalme, lakini bado hajafahamu ni lini atakapozuru anachofikiria kuwa nchi mpya zaidi ulimwenguni.

Itabidi Misri, Sudan na Umoja wa Mataifa kutambua 'Ufalme wa Sudan' kabla hajakuwa rasmi bintiye mfalme.