Yadaiwa ndege ya Malaysia ilishambuliwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ndege hii ilikuwa inatoka Amsterdam kuelekea Kualar Lumpur

Maafisa nchini Ukraine wanasema kuwa ndege ya abiria iliyoanguka nchini humo ilidunguliwa katika eneo la mashariki mwa taifa hilo ambako waasi wanaoiunga mkono Urusi wamekuwa wakipigana na vikosi vya serikali.

Wanasema abiria wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo ya shirika la Malaysia iliyokuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kuelekea Kualar Lumpur wamefariki.

Wengi wa abiria hao walikuwa ni raia wa Uholanzi.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alitaja tukio hilo kama kitendo cha ugaidi.

Maafisa wa Ukraine walichapisha kile walichotaja kuwa mawasiliano ya simu yaliyonaswa kati ya waasi wakiwaeleza maafisa wa Urusi kwamba ni wao ndio waliohusika katika kuindungua ndege hiyo.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Ukraine, Pavlo Klimkin, amesema kuwa serikali ina ushahidi wa kutosha kwamba ndege hiyo ilidunguliwa.

'Je waasi walihusika?'

'Tulinasa pia mawasiliano ya simu kati ya magaidi hao wakizungumzia kundunguliwa kwa ndege hiyo.Kwa sasa tunatafsiri sauti zao na kisha tutaziweka kwenye mtandao wa internet ili kuthibitisha hilo."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mabaki ya ndege ya Malaysia iliyodunguliwa

Hata hivyo sauti hizo zilizonaswa bado hazijathibitishwa na upande uliohuru na waasi hao wamekanusha kuhusika wakisema kuwa ni wanajeshi wa serikali ndio walioidungua ndege hiyo.

Kadhalika marekani imesema kuwa inaamini ndege hiyo ililipuliwa angani na wala halikuwa tukio la ajali.

Makamu wa rais Joe Biden hata hivyo amesisitiza kuwa Marekani bado inatafuta maelezo.

''Ndege ya Malaysia iliyokuwa ikitoka Ulaya magharibi kuelekea Kuala Lumpur, yaelekea ilipokuwa ikivuka karibu na mpaka kati ya Ukraine na Urusi, nasema yaelekea kwa sababu hatuna taarifa za kina, nataka kuwa makini na kile ninachosema yaelekea ilidunguliwa, ilidunguliwa na wala sio ajali. Ililipuliwa kutoka angani. Tunaona ripoti kwamba huenda raia wa Marekani walikuwa kwenye ndege hiyo na bila shaka huo ndio wasiwasi wetu wa kwanza.''

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema kuwa Ukraine inapaswa kuwajibika katika tukio la udunguaji wa ndege hiyo.

Msemaji wa serikali ya Urusi amesema kuwa mkasa huo haungetokea ikiwa Kiev haingeimarisha harakati zake za kijeshi mashariki mwa Ukraine.