Urusi na Ukraine zatupiana lawama

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk

Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk amesema kuwa kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia ni uhalifu wa kimataifa unaopaswa kupelelezwa na mahakama ya jinai iliyoko The Hague.

Waziri huyo mkuu amesema kuwa mauwaji hayo yametekelezwa na Serikali ya Urusi, huku Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akirushia lawama Ukraine.

Naye Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amesema kuwa ajali hiyo ya ndege ilionekana kuwa tendo la Ugaidi, kwani inaonekana ilishambuliwa na waasi wanaofadhiliwa na Urusi.

Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amesema nchi yake inaomboleza vifo vya zaidi ya watu 150, raia wa taifa lake walioangamia katika ajali ya ndege ya Malaysia iliyodunguliwa Nchini Ukraine.

Image caption Lawama zimekuwa zikirushwa kati ya Ukraine na Urusi

Anasema kuwa kulikuwa na waholanzi 154 kwenye ndege hiyo.

Kati ya walioabiri ndege hiyo, kulikuwemo takriban watafiti 100 wa ugonjwa wa ukimwi, wafanyikazi katika idara ya afya na wanaharakati waliokuwa wanasafiri ughaibuni kuhudhuria mkutano wa kimataifa huko Melbourne.

Aliyekuwa rais wa Jamii ya Kimataifa inayoshughulikia maswala ya ugonjwa wa Ukimwi, Joep Lange anadhaniwa kuwa mmoja wa walioabiri ndege hiyo.