Waangalizi wa Ulaya wazuiliwa Ukraine

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ndege ya Malaysia ilioanguka mashariki mwa ukraine

Waangalizi wa muungano wa Ulaya waliotumwa katika eneo linalodhibitiwa na waasi mashariki mwa Ukraine ambapo ndege ya Malaysia Airline iliangushwa kwa kupigwa kombora siku ya alhamisi wamesema kuwa watu waliojihami wamewanyima rukhsa ya moja kwa moja kuona mabaki ya ndege hiyo.

Msemaji wa shirika la usalama na ushirikiano wa ulaya amesema kuwa kundi lao lilikabiliana na wapiganaji hao wengine wakiwa wamelewa kabla ya mmoja wao kufyatua risasi hewani.

Baada ya saa moja ,waangalizi hao 25 waliondoka kwa kushindwa kubuni eneo ambalo makundi ya wataalam wangetumia kuchunguza kuanguka kwa ndege hiyo mbali na kuiondoa miili ya takriban abiria 300 na wafanyikazi wa ndege hiyo.