UN:Mapigano yaendelea Sudan Kusini

Haki miliki ya picha AFP

Umoja wa mataifa umesema kumekuwepo kwa siku mbili za mapigano katika mji wa Nasir, Sudani ya Kusini.

Msemaji wa Umoja wa matifa amesema vikosi vya waasi vimeyakalia maeneo ya katikati ya mji huo ambao mapema mwaka huu ulitumika kama makao makuu ya muda ya kiongozi wa waasi Riek Machar.

Shirika la Habari la Reuters linaripoti kuwa kambi ya waasi wa Sudani Kusini imesema inatuma ujumbe Ujumbe wake kuelekea nchini Uganda kufanya mazungumzo na Rais Yoweri Kaguta Museveni ili kumwomba Museveni kuondoa vikosi vyake vya kijeshi katika Sudani Kusini ambako vilipelekwa kuisaidia serikali ya Juba.

Mwezi Januari Rais Museveni alisema vikosi vyake vinamuunga mkono rais wa Sudan Salva Kiir dhidi ya waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar.

Uwepo wa vikosi vya kijeshi vya Uganda katika Sudani Kusini umelalamikiwa mara zote na waasi. Nchi nyingine jirani pamoja na mataifa ya nje yana mashaka kuwa uwepo wa vikosi hivyo unachelewesha juhudi za kuondoa msuguano ulioanza miezi saba iliyopita kiasi cha kuipeleka nchi katika njaa kali.

Hata hivyo Uganda imeendelea kuweka msimamo wake kuwa kuondoa vikosi vyake kutatokana na uganda yenyewe kuamua na sio amri ya mtu mwingine yeyote.

Mada itakayozungumzwa tunategemea itafungua ukurasa mpya na Rais Mseveni, anasema Miyong Kuon msemaji wa Machar alipokuwa Adis Ababa ambako mazungumzo ya Amani yalikuwa yakiendelea.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uganda Fred Opolot hakutoa maelezo ya kina juu ya mazungumzo lakini amesema mazungumzo hayo kiujumla yatahusu kutafuta njia ya kujikwamua katika hali iliyopo hivi sasa ili kuelekea katika kupata suluhu. Kumekuwa na mazungumzo ya kutafuta Amani tangu kulipoibuka msuguano kati ya pande hizo mbili ndani ya sudani kusini lakini kumekuwa na maendeleo yasiyoridhisha.