Ebola:Daktari adhurika Sierra Leone

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jitihada zinahitajika kupambana na ugonjwa wa Ebola

Daktari aliyekua akiongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone anapatiwa matibabu ili kupambana na Virusi vya ugonjwa huo, Taarifa kutoka Ofisi ya Rais imeeleza.

Sheik Umar Khan alibainika kuwa na Virusi vya Ebola na sasa amelazwa katika hospitali moja mjini Kailahun ambapo ugonjwa huo umekua ukijitokeza kwa wingi.

Zaidi ya Watu 630 wamepoteza maisha katika nchi tatu za Afrika magharibi tangu mlipuko wa ugonjwa huo kuanza nchini Guinea mwezi Februari, takwimu za Umoja wa Mataifa zimeonesha.

Taarifa kutoka Ikulu ya nchi hiyo zimesema Waziri wa Afya alikua akibubujikwa na machozi aliposikia taarifa za dokta Khan.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ugonjwa wa Ebola umekua tishio katika ukanda wa Afrika magharibi

Waziri wa Afya wa Sierra Leone Miatta Kargbo amemuita daktari huyo kuwa “shujaa wa taifa” na kusema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha anapona.

Mwandishi wa BBC wa mjini Freetown amesema wauguzi kadhaa katika hospitali ya Serikali mjini Kenema ambako kuna tishio kubwa la ugonjwa wa Ebola waligoma siku ya jumatatu baada ya wenzao watatu kupoteza maisha kwa kile kilichohisiwa kuwa ugonjwa wa Ebola.

Mgomo huo ulisitishwa baada ya Serikali kusikiliza madai yao, ikiwemo kuhamisha wodi yenye wagonjwa wa Ebola kutoka hospitali na Operesheni ya kupambana na ugonjwa huo kuchukuliwa na Shirika la madaktari wasio na mipaka, Medicins Sans Frontieres.

Jumamosi Shirika la afya duniani lilisema katika idadi ya 632 waliopoteza maisha Afika magharibi kutokana na Ebola,watu 206 ni kutoka nchini SierraLeone