AlShabab yaua mama kutofunga niqabu

Haki miliki ya picha Reuters

Wanamgambo wa kiislamu wa Al Shabab wamempiga mwanamke mmoja risasi na kumuua kwa kukosa kujifunga niqab kichwani.

Jamaa za mwanamke huyo mwenyeji wa mji wa Hosingow kusini mwa Somalia wanasema mwanamke huyo alikataa kujifunika kitambaa kichwani kuambatana na sheria za dini ya kislamu .

''alikuwa ameonywa ajisitiri lakini wapiganaji hao waliporejea wakashikwa na hasira walipopata kuwa hakuwa amejifunika na hivyo wakampiga risasi''.

Image caption Al Shabab yaua mama kwa kukosa Niqab

Jamaa zake wameiambia BBC kuwa Ruqiya Farah Yarow alikuwa amewafokea wapiganaji hao akiwataka waondoke kwake na kusema kuwa angejisitiri baadaye.

Kundi la Al Shabab linalomiliki asili mia kubwa ya maeneo ya Kusini na Katikati ya Somalia na limekuwa likishinikiza kutumiwa kwa sheria kali za kiislamu.

Hata hivyo msemaji wa kundi hilo amekanusha kuwa ni wao waliomuua mwanamke huyo .

Msemaji huyo anasema kuwa licha ya kudhibiti maeneo makubwa nchini humo kundi hilo bado halijatoa maelezo ya vipi wanawake wanastahili kujisitiri.