Libya:Uingereza kuufunga ubalozi wake.

Image caption Ubalozi wa Uingereza mjini Tripoli,Libya

Uingereza inatarajiwa kuufunga ubalozi wake kwa mda katika mji mkuu wa Tripoli nchini Libya kufuatia mapigano makali katika mji wa Benghazi.

Zaidi ya watu mia mbili wameuawa katika miji hiyo miwili katika kipindi cha majuma mawili yaliopita.

Wizara ya maswala ya kigeni nchini Uingereza imesema kuwa oparesheni za ubalozi huo zitasitishwa baada ya siku ya jumatatu.

Imesema kuwa inafanya mipango ya kuwaondoa raia wa Uingereza ambao wanataka kuondoka nchini humo.

Mataifa mengi ya Magharibi ikiwemo Marekani tayari yamewaondoa wajumbe wao.

Siku ya ijumaa maelfu ya waandamanaji walifanya maandamano katika barabara za mji wa Tripoli na Benghazi ili kuwapinga wapiganaji ambao wamekuwa wakikabiliana na vikosi vya serikali ya Libya.