Kobe mwenda mbio akamatwa Marekani

Image caption Kobe huyu anasemekana alitoroka kwa hofu ya kukamatwa na polisi

Polisi mjini Los Angeles Marekani wamefanikiwa kumshika tena Kobe mkubwa aliyetoroka baada ya kinachoelezewa kama harakati ndogo za kumkimbiza Kobe huyo katika barabara za mji huo.

"Kobe huyo alijaribu kukimbia lakini maafisa wetu walikua na mbio zaidi," ilinukuu taarifa ya idara ya polisi ya Alhambra kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Idara ya polisi ya mtaa huo imesema kuwa kobe huyo alijaribu kutoroka lakini maafisa wa polisi walikimbia kwa haraka zaidi na kumkamata.

Maafisa wawili wa polisi walifanikiwa kumbeba mnyama huyo na kumuweka ndani ya gari la polisi.

Kobe huyo kwa jina Clark alipelekwa katika kituo cha wanyama waliookolewa ambapo hatimaye alijiunga na wamiliki wake.

Kumfuga mnyama huyo bila ya idhini ya maafisa wakuu ni kinyume na sheria, lakini polisi hawatawafungulia mashitaka wamiliki wake.

Kobe wana uwezo wa kukimbia kasi ya kilomita 1.6 kwa saa ikiwa wanataka.