Jela kwa kuwauzia watu Mvinyo bandia

Image caption Bwana Kurniawan alipatikana na hatia ya kuuza Mvinyo bandia wenye thamani ya dola milioni 20

Mwanamume aliyewalaghai watu kwa kuwauzia mvinyo bandia, Rudy Kurniawan, 37, amefungwa jela kwa miaka kumi na kuamrishwa kulipa faini ya dola milioni 20 kwa kosa hilo.

Rudy aliuza Mvinyo ghushi wenye thamani ya mamilioni ya dola bila ya kujulikana kwa miaka mingi.

Pia ameamrishwa kulipa dola milioni 28.4 kwa waathiriwa wanaojumuisha tajiri William Koch.

Bwana Kurniawan ni mtu wa kwanza kuwahi kwenda jela kwa kuuza mvinyo bandia nchini Marekani.

Alipatikana na hatia ya kuchanganya mvinyo wa zamani na mvinyo wa mpya nyumbani kwake. Baada ya kuinchanganya aliuza Mvinyo huo kwa bei ghali mno akidai kuwa ni Mvinyo wa kipekee.

Vibandiko bandia alivyotumia bwana Kurniawan kuwahadaa waekezaji kununua bidhaa zake vilipatikana nyumbani kwake.

Kashfa hii aliifanya tangu mwaka 2004 hadi 2012 kulingana na viongozi wa mashitaka.

Mwezi Disemba alipatikana na hatia ya kuwalaghai watu kwa nja ya posta.

Kama raia wa Indonesia, Bwana Kurniawan atarejeshwa nchini Indonesia ili akafunguliwe mashitaka huko. Tayari amekuwa jela kwa miaka 2 tangu kukamatwa mwaka 2012.

Mnamo mwaka 2006, inaaminika kwamba aliuza chupa 12,000 za mvinyo bandia katika mnada.

Lakini maafisa wakuu walisema kuwa walipata maelfu ya vibandiko vya mvinyo mzuri zaidi wa Burgundy na Bordeaux pamoja na chupa ambazo hazikuwa zimwekwa vifuniko nyumbani kwake.