Maelfu waandamana kupinga vita Gaza

Maandamano ya London kuhusu Gaza Haki miliki ya picha bbc

Maelfu ya watu wameandamana mjini Cape Town, Afrika Kusini, London na kwengineko kupinga mashambulio ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza.

Maandamano ya Afrika Kusini yaliitishwa na National Coalition for Palestine, inayojumuisha makundi ya kidini, jamii, vyama vya wafanyakazi na vyama vya kisiasa.

Inafikiriwa kuwa maandamano hayo yalikuwa kati ya maandamano makubwa kabisa kufanywa katika mji huo tangu ubaguzi wa rangi kumalizika Afrika Kusini.

Kati ya watu waliohudhuria ni askofu wa zamani wa Cape Town aliyepata tuzo ya Nobel ya amani, Desmond Tutu.

Maandamano piya yamefanywa mjini London, Uingereza na Sydney, Australia.

Gaza kwenyewe, Israil imeendelea kuishambulia baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kumalizika Ijumaa asubuhi.

Imetokea miripuko miwili mikubwa katika eneo la bandari ya Gaza.

Mwandishi wa BBC anasema inafikiriwa kuwa shambulio moja lililenga eneo la mafunzo la Hamas.

Wapalestina wanasema watu kama watano wameuwawa tangu mapigano kuanza tena pamoja na mfuasi mwandamizi wa Hamas.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa nyumba za watu karibu 65,000 wa Gaza zimeangamia katika mashambulio ya karibuni.

Kundi la Hamas limekataa kuzidisha muda wa kusitisha mapigano kwa sababu linasema madai yao kuwa vizuizi vilioko dhidi ya eneo la Gaza viondoshwe bado hayakutekelezwa.

Lakini inavofahamika ni kuwa mazungumzo baina ya Hamas na wapatanishi wa Misri yanaendelea.