Waziri mkuu mpya ateuliwa CAR

Rais Catherine Samba-Panza wa CAR Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Bi Samba Panza

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-Panza, amemteua Muislamu kuwa waziri mkuu mpya.

Mahamat Kamoun, ambaye alikuwa mshauri maalumu wa Michel Djotodia, kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Seleka, ataongoza serikali ya mpito.

Waandishi wa habari wanasema hatua hiyo ni jaribio la kuunda serikali ya pamoja baada ya ghasia za kidini za zaidi ya mwaka mmoja.

Tangazo hilo lilitolewa kwenye redio ya taifa na msemaji wa rais ambaye mwenyewe ni Mkristo.

Ghasia zilizuka baina ya Wakristo na Waislamu baada ya wapiganaji wa Seleka, wengi wao waliokuwa Waislamu, walipomtoa madarakani Rais Francois Bozize mwaka jana.