Mkuu wa polisi auawa nchini Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kanali Muhammad Suwaysi aliteuliwa kama mkuu wa polisi mjini Tripoli mwaka 2012

Mkuu wa polisi katika mji mkuu wa Libya Tripoli, ameuawa na watu wasiojulikana.

Kanali Muhammad Suwaysi alipigwa risasi, alipokuwa anaondoka kwenye mkutano katika eneo la Tajoura , mtaa ulio mashariki mwa mji mkuu Tripoli.

Wenzake wawili walitekwa nyara kwa mujibu wa taarifa za wizara ya ndani.

Libya imekumbwa na vurugu zinazosemekana kusababishwa na wapiganaji wa kiisilamu, ambao walisababisha harakati za kumuondoa mamlakani Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Maelfu ya watu wamelazimika kutoroka Tripoli.

Zaidi ya miaka mitatu baada ya kuondolewa mamlakani kwa Gadaffi, jeshi la polisi nchini Libya linasemekana kuwa dhaifu, ikilinganishwa na wapiganaji wanaodhibiti sehemu kubwa za nchi hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji wa kiisilamu ambao wamekuwa wakizua vurugu nchini Libya

Afisa huyo aliuawa wakati alipokuwa anatoka katika mkutano na maafisa wa mtaa wa Tajoura.

Maafisa wengine wawili waliokuwa naye, walitii masharti ya washambuliaji na kuondoka kwenye gari lao huku wakitekwa nyara.

Mamia ya watu wamefariki katika miezi ya Julai na Agosti katika kile kinachoonekana kuwa kukithiri kwa vurugu.